Meya wa Jiji la Dar es salaam, Issaya Mwita amesema kwamba hafikirii kuhama Chadema kwani familia yake itateketezwa kwa mapanga na wananchi.
Mwita amesema kwamba amekitumikia Chadema kwa muda mrefu ikiwepo kutumia fedha zake binafsi kwenye kukijenga chama hivyo hadhani kama anaweza kuhamia chama kingine kwani hata madaraka aliyonayo anaamini yanamtosha kabisa.
Mwita amesema kwamba amesikitika sana kuona kuna baadhi ya watu waliohama vyama na kuongeza kwamba yeye ameaminiwa na wana Dar es salaam ndiyo maana akapewa dhamana kubwa ambayo ni kubwa kuliko hata nafasi ya Waziri.
Pia Mwita amesema kwamba sifa moja ya kabila analotoka siyo watu wa kuyumbishwa hivyo siku atakapobadili msimamo ndiyo siku ambayo ataipoteza familia na yeye mwenyewe.
Mwita ameongeza kwa kusema kwamba aina yake ya kuliongoza jiji la Dar es salaam imekuwa tofauti sana kwani ameamua kuwa mkimya ili kuleta maendeleo kwa wananchi hivyo suala la kupiga kelele halitakuwa na tija kama hakutakuwa na maendeleo.