Rais wa Marekani, Donald Trump ameiorodhesha Korea Kaskazini kuwa taifa linalofadhili ugaidi miaka tisa baada ya kuondolewa katika orodha hiyo.
Katika mkutano wa baraza la mawaziri rais Trump amesema kuwa hatua hiyo itasababisha kuwekwa kwa vikwazo vikali dhidi ya taifa hilo vinavyotarajiwa kutangazwa siku ya Jumanne.
Lakini waziri wa maswala ya kigeni Rex Tillerson baadaye alikiri kwamba madhara yake hayatakuwa makubwa.
Trump amelaumu mpango wa kinyuklia wa taifa hilo na ufadhili wa kile amekitaja kuwa vitendo vya ugaidi wa kimataifa.
Akitoa uamuzi huo katika ikulu ya Whitehouse , Trump amesema kuwa hatua hiyo ingetekelezwa kitambo.
Mnamo mwezi Septemba , Marekani ilipendekeza idadi kadhaa ya vikwazo vya Umoja wa kimataifa dhidi ya Korea Kaskazini, ikiwemo marufuku ya mafuta mbali na kupigwa tanji kwa mali ya rais wa taifa hilo Kim Jong Un.
Hatua hiyo inafuatia majaribio masita ya makombora ya kinyuklia yaliotekelezwa na Korea Kaskazini.
Korea Kaskazini sasa inajiunga na Iran , Sudan na Syria katika orodha ya mataifa ambayo yanadaiwa kufadhili ugaidi wa kimataifa.
Taifa hilo lilikuwa katika orodha hiyo awali lakini likaondolewa 2008 na utawala wa rais George W Bush ikiwa miongoni mwa majadiliano kuhusu mpango wa kinyuklia wa Korea Kaskazini.
Lakini kampeni ya kulirudisha miongoni mwa mataifa yanayofadhili ugaidi wa Kimataifa iliishika kasi baada ya mwanafunzi wa Marekani Otto Wambier kuuawa muda mfupi baada ya kuachiliwa kutoka kwa kizuizi cha Korea Kaskazini.
Lakini hatua hiyo ya kuirudisha Pyongyang katika orodha ya mataifa yanayofadhili ugaidi itarudisha nyuma uwezekano wa kuanzisha mazungumzo na taifa hilo.