Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji amesema chama hakina mgogoro na aliyekuwa Mwenyekiti wa Bavicha, Patrobas Katambi ambaye ametangaza kujiunga na CCM.
Mashinji amesema kuwa haoni sababu ya kumzuia mtu kuondoka kwa kuwa mtu anapoamua kwenda sehemu yoyote anakuwa na matarajio.
Pia Dk Mashinji amesema anamtakia heri (Katambi) na kuwataka CCM kumtumia katika sehemu ambavyo wanaona anafaa kutumika kwa faida ya Watanzania wote.
“Hatuna mgogoro wowote na kimsingi mimi nimtakie tu heri (Katambi) na wakipenda (CCM) wamtumie kwenye eneo watakaloona anafaa kutumika kwa faida ya Watanzania wote,”.
Hata Hivyo, Dk Mashinji amesema kuwa walikuwa wanamuandaa Katambi asaidie chama hicho kwenye kitengo cha sheria.
Katambi ametangaza leo kujiunga na CCM mbele ya Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) unaofanyika katika Ukumbi wa Ikulu jijini Dar es Salaam.