Manchester United inatarajia kuingia sokoni kunasa saini ya mshambuliaji mmoja ili kuimarisha kikosi hicho.
Majina yanayotajwa kuwindwa na Man United ni Antoine Griezmann wa Atletico Madrid na Gareth Bale anayecheza Real Madrid.
Hata hivyo, kocha wa Man United, Jose Mourinho hajui atamsajili mchezaji gani kati ya Griezmann au Bale .
Washambuliaji wote wanamvutia Mourinho na atalazimika kuchagua mmoja ili kwenda kuongeza kasi katika safu ya ushambuliaji Man United.
Mourinho ana Romelu Lukaku na Zlatan Ibrahimovic aliyerejea uwanjani akitokea katika maumivu ya goti yaliyomuweka nje ya uwanja miezi saba.
Mshambuliaji Griezmann na Bale mmoja kati yao anapewa nafasi ya kuvaa uzi wa Man United katika dirisha la usajili Januari, mwakani endapo mpango huo utafanikiwa mapema kabla ya majira ya kiangazi.
Bale amekuwa na maisha magumu Real Madrid baada ya kuandamwa na majeraha ya mara kwa mara, lakini Griezmann tangu kuanza msimu huu hayuko fiti.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa, amefunga mabao mawili katika mechi 10 alizocheza na mwishoni mwa wiki iliyopita alizomewa na mashabiki wa Atletico Madrid katika mchezo dhidi ya mahasimu wao Real Madrid.
Msimu uliopita Griezmann alicheza kwa kiwango bora na aliwekwa sokoni akiuzwa Pauni 200 milioni, lakini Man United ilishindwa kumsajili baada ya Atletico Madrid kufungiwa na Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) kusajili.