Kamishna mkuu wa Mamlaka Kuzuia na Kupambana na Madawa ya Kulevya, Rogers Siyanga amefafanua marekebisho ya Sheria Namba 5 ya mwaka 2017 ya kudhibiti na kupambana na madawa ya kulevya.
Amesema hayo mbele ya waandishi wa habari kwenye ofisi ya Mamlaka hiyo iliyopo Upanga jijini Dar es Salaaam.
Siyanga amesema kuwa miongoni mwa vipengele vilivyorekebishwa ni kile cha wauza madawa ya kulevya wakubwa kutupwa jela kifungo cha maisha huku wale wadogo wakikabiliwa na adhabu ya miaka 30 jela.
Kamishna huyo amesema kuwa lengo la marekebisho hayo ya sheria yaliyofikiwa kwenye kikao cha bunge kilichopita, ni kuboresha utekelezaji wa sheria hiyo na kuondoa upungufu uliojitokeza wakati wa utekelezaji wa majukumu ya mamlaka hiyo.
Pia ameongeza kwa kusema kuwa vipengele vingine vilivyoboreshwa ni pamoja na kile kinachoipa mamlaka hiyo uwezo wa kupata taarifa kutoka vyanzo mbalimbali kama kwenye taasisi za serikali na kuwa na uwezo wa kutumia silaha pale inapobidi.
Vipengere vingine vilivyorekebishwa ni pamoja na sheria kuongeza fursa kwa watumiaji wa madawa ya kulevya kupata matibabu na huduma nyingine badala ya kuhukumiwa kifungo gerezani.