Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe amesema kuwa yupo tayari kuachia madaraka ila ahakikishiwe usalama wake na mali zake.
Mugabe amekubali kuachia madaraka lakini kwa masharti kuwa yeye na mkewe Grace Mugabe wapatiwe kinga ya kudumu na mali zake binafsi zisiharibiwe baada ya kujiuzulu.
Rais Mugabe ameshawasilisha masharti hayo kwa njia ya barua na tayari Jeshi la nchi hiyo limekubaliana nayo.
Chama cha Zanu PF leo kimetangaza kukutana na wabunge, Mawaziri na Maseneta wa Chama hicho mchana huu.
Taarifa hizo zilizovujishwa na watu wa karibu wa Rais Mugabe zimetoka wakati huu ambapo Rais Mugabe alishurutishwa na Chama chake jana jumapili kutangaza kujiuzulu nafasi yake ya urais wa nchi hiyo.
Hata hivyo bado haijabainika kuwa ni lini kiongozi huyo ataachia madaraka rasmi kwani leo Jumatatu alitakiwa kutangaza kujiuzulu nafasi hiyo ya urais.