Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema iwapo Sheria Namba Tano ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992 itawasilishwa bungeni wa ajili ya kupitishwa watakuwa tayari kufa kuliko kukubali ipitishwe.
Akizungumza jana Jumanne jioni wakati wa kumnadi Mgombea Udiwani wa Kata ya Ibhigi, iliyopo Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya, Emmanuel Simba, Mbowe amesema kama kuna wakati wanaume wanatakiwa kusimama wahesabiwe ni wakati huo.
Amesema kupitisha sheria hiyo maana yake ni kuingiza ubatili walioufanya ili uwe sheria kamili, kwamba hakuna mikutano ya vyama vya siasa, hakuna majadiliano ya mustakabali wa nchi.
Mbowe ambaye ni Mbunge wa Hai alisema watalikataa hilo ili watoto watakaokuja kesho na keshokutwa wajue baba na mama zao walipambana kulipigania Taifa lao.
Amesema Watanzania kwa umoja wao wasilikubali hilo kwa sababu litawanyima haki kukutana na kujadili wanataka nini kifanyike na watakuwa wamekubali kurudi nyuma miaka mitano.
Kuhusu Tume ya Taifa ya Uchaguzi iliyokutana juu na wawakilishi wa vyama vya siasa , ambapo ilitoa tamko kuwa katika kampeni za uchaguzi wa marudio ya udiwani, wasijadili masuala ya siasa nje ya kata, jambo ambalo ni la kipuuzi.
Mbowe pia alizungumzia kashfa zinazodaiwa kufanywa na aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu alipokuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, amesema kama wana uhakika na tuhuma hizo wampeleke mahakamani.