Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Seleman Jafo amezindua kampeni ya “Mkoa wetu, Viwanda vyetu” yenye lengo la kuanzisha viwanda 100 katika kila Mkoa nchini, jana Mjini Dodoma.

Akizungumza katika uzinduzi huo Mhe. Jafo alisema kuwa ni jambo lililowazi kuwa ili nchi iweze kuendelea inahitaji kufanya mapinduzi makubwa katika viwanda.

“Historia ya Viwanda siyo ngeni katika nchi yetu, tangu tupate Uhuru mwaka 1961 Serikali imekuwa ikilenga katika kujenga Uchumi kupitia Viwanda ambapo tokea wakati huo viwanda vingi vidogo vya kati na vikubwa vilianzishwa na kusimamiwa huku sehemu kubwa ya viwanda hivyo vikisimamiwa na Serikali” alieleza Mhe. Jafo.

Aidha alisema kuwa ili azma hiyo iweze kufikiwa TAMISEMI itashirikiana na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji katika kuweka mazingira wezeshi pamoja na kutoa mwongozo wa namna ya kushirikisha Tasisi za Serikali na Sekta Binafsi na wadau wa maendeleo katika kuanzisha, kuendesha na kusimamia Viwanda ili kuikuza sekta hiyo nchini.

“TAMISEMI kupitia Mikoa na Halmashauri imedhamiria kutekeleza kwa vitendo azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga Uchumi wa Viwanda, hivyo kila Mkoa uanishe Viwanda vya vipaumbele kwa kuzingatia Malighafi muhimu za Viwanda zinazopatikana kwenye maeneo yao pamoja na mahitaji muhimu ya soko” alifafanua Mhe. Jafo.

Hata hivyo, Mhe. Jafo aliwataka Wakuu wa Mikoa, wakuu wa Wilaya na Halmashauri kuwatumia ipasavyo Maafisa Maendeleo ya Jamii na Maafisa Ugani ili kuwahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa viwanda nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *