Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu upande wa watoto imetupilia mbali kesi iliyofunguliwa na mwanamitindo Hamisa Mobeto dhidi ya mwanamuziki Naseeb Abudul ‘Diamond Platmunz’ kuhusu matunzo ya mtoto.
Uamuzi huo umetolewa leo mbele ya Hakimu Devotha Kisoka baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili ukiwemo wa Diamond ambaye aliwasilisha pingamizi dhidi ya kesi hiyo.
Hakimu Kisoka amesema kuwa anakubaliana na hoja za upande wa mlalamikiwa kwamba kulikuwa na upungufu katika ufunguaji wa kesi hiyo.
Katika pingamizi lake Diamond amedai kuwa kesi hiyo ilifunguliwa kwa kutumia kifungu ambacho si sahihi hata hivyo hoja hiyo ilipingwa na mawakili wa Hamisa Mobeto.
Mobeto alifungua kesi hiyo mahakamani hapo kwa kuiomba mahakama imuamuru Diamond atoe matunzo ya moto waliozaa.
Hamisa alitaka mahakama hiyo imuamuru Diamond atoe matunzo ya mtoto ya kila mwezi ya shilingi milioni 5.
Pia Mobeto alitaka Diamond amuombe msamaha kwa kumsababishia madhara yaliyoshtua familia yake.
Diamond aliwasilisha hati ya kupinga madai hayo akidai kuwa gharama za kulipa milioni 5 kila mwezi kwa ajili ya matunzo ya mtoto hawezi kuzimudu.