Baada ya wanafunzi kuandamana katika ofisi za Bodi ya Mikopo (HELSLB) kudai mikopo, jeshi la kutuliza ghasia (FFU) wamelazimika kuweka kambi kusambaratisha maandamano hayo.

Wanafunzi hao walikusanyika jana katika ofisi hizo za HESLB zilizoko Mwenge, Dar es Salaam, wakishinikiza wapewe mikopo ili wafanye usajili kwa mwaka wa masomo wa 2017/18.

Baada ya kukusanyika ndani ya ofisi hizo, huku wakilalamika wapewe mikopo hiyo, ndipo askari hao wa FFU waliwaamuru kutoka nje ya geti.

Wiki iliyopita, Serikali iliidhinisha tsh bilioni 427 za mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2017/18, huku viongozi wa wanafunzi wakilalamika kuwa bajeti hiyo ni ndogo ukilinganisha na mahitaji yao.

Akitoa ufafanuzi kwa hilo, Naibu Waziri wa Elimu, William ole Nasha, amesema Serikali imetenga fedha hizo kulingana na maombi ya Bodi ya Mikopo (HESLB).

Bw. Nasha amesema kwa kuzingatia hilo, ndiyo maana tayari Sh bilioni 147 za robo ya kwanza ya mwaka wa masomo 2017/18 zimeshaingizwa kwenye akaunti ya HESLB.

Mkurugenzi wa Idara ya Haki na Wajibu wa Wanafunzi kutoka Mtandao wa Wanafunzi Tanzania, Abdul Nondo, amesema inashangaza kwa wanafunzi wengi kukosa mikopo wakati walitimiza vigezo vyote.

Hata hivyo, Meneja Habari, Elimu na Mawasiliano wa HESLB, Omega Ngole, amesema tayari wameyapokea malalamiko yao na wamewaambia waandike majina yao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *