Tume ya uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imetangaza kwamba uchaguzi mkuu nchini humo sasa utafanyika Desemba 2018.

Hatua hiyo hata hivyo haijaufurahisha upinzani ambao unataka Rais Joseph Kabila aondoke madarakani.

Uchaguzi ulipangiwa kufanyika mwaka huu chini ya makubaliano yaliyoafikiwa mwaka jana, lakini tume ya uchaguzi imechelewa kuandaa uchaguzi.

Awali, ilikuwa imetangaza kwamba uchaguzi unaweza tu kufanyika mwaka 2019.

Lakini sasa tume hiyo imetangaza kwamba uchaguzi wa rais, wabunge na viongozi wa serikali za majimbo utafanyika mnamo 23 Desemba, 2018.

Upinzani umesisitiza kwamba ni sharti Rais Kabila aonondoke madarakani kufikia mwisho wa mwaka huu.

Afisa wa tume ya uchaguzi Jean-Pierre Kalamba amesema matokeo ya muda yatatangazwa katika kipindi cha wiki moja baada ya upigaji kura kufanyika, mnamo tarehe 30 Desemba, lakini matokeo kamili yatatangazwa tarehe 9 januari, 2019.

.Tume ya uchaguzi ilikuwa imesema haiwezekani kuandaa uchaguzi kwa wakati kutokana na matatizo ya kuandaa sajili ya wapiga kura, hasa eneo lenye misukosuko la Kasai katikati mwa nchi hiyo.

Tangazo la Jumapili limetolewa siku kumi baada ya ziara ya balzoi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *