Watu 26 wameuawa kwa kupigwa risasi na mtu mwenye silaha aliyewafyatulia risasi waumini katika kanisa moja jimbo la Texas wakati wa ibada.
Shambulio hilo lilitekelezwa katika kanisa la First Baptist Church katika mji wa Sutherland Springs, mji mdogo katika wilaya ya Wilson, Texas.
Mshambuliaji, ambaye anadaiwa kuuawa baada ya kutekeleza mauaji hayo, aliingia kanisani na kuanza kuwafyatulia risasi watu mwendo wa saa tano unusu asubuhi.
Gavana Greg Abbott amethibitisha idadi ya waliofariki na kusema ndicho kisa kibaya zaidi cha mauaji ya kutekelezwa kwa kutumia bunduki katika historia ya texas.
Mkuu wa idara ya usalama wa Texas Freeman Martin amesema waathiriwa walikuwa na umri wa kati ya miaka 5 na 72.
Maafisa wamesema watu zaidi ya 20 pia walijeruhiwa na wamelazwa hospitalini.
Bw Martin amesema mshukiwa ni mwanamume mzungu wa umri wa miaka 20 ambaye alikuwa amevalia mavazi meusi na fulana ya kujikinga dhidi ya risasi pamoja na kuwa na bunduki yenye uwezo mkubwa.
Alianza kufyatua risasi nje ya kanisa kabla ya kuingia ndani na kuendelea kufyatulia watu risasi.
Mwenyeji “litwaa bunduki yake na kuanza kumfyatulia ” risasi mshukiwa kabla ya mshukiwa huyo kutoroka akitumia gari.
Raia huyo alimwandama mshukiwa huyo ambaye aliendesha gari lake na kisha kuliangusha katika barabara wilaya ya Guadalupe.
Haijabainika iwapo alifariki kutokana na majeraha ya risasi aliyojisababishia mwenyewe au kutokana na mejaraha kutoka kwa raia huyo, Martin ameongeza.
Mshukiwa ametajwa kuwa Devin P Kelley, 26, kwa mujibu wa vyombo vya jhabari Marekani.
Mhubiri wa kanisa hilo la First Baptist Frank Pomeroy, ameambia ABC News kwamba binti yake wa miaka 14 kwa jina Annabelle ni miongoni mwa waliouawa.
Sutherland Springs ni mtaa mdogo wenye wakazi wasiozidi elfu moja ambao hupatikana kilomita 50 hivi kusini mashariki mwa mji wa San Antonio mjini Texas.
Maafisa wa FBI kutoka San Antonio wametumwa kufanya uchunguzi lakini kufikia sasa lengo la mshambuliaji halijabainika.