Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mohammed Enterprises (MeTL Group), Mohammed Dewji amepongeza uamuzi wa Rais wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda kwa kufufua viwanda ambavyo vilikuwa havifanyi kazi.

Dewji ametoa pongezi hizo wakati akizungumza katika mkutano wa siku mbili wa Global Business Forum 2017 (GBF) kuhusu Viwanda kwa Nchi za Afrika uliofanyika Dubai, Falme za Kiarabu (UAE).

Mfanyabiashara huyo ambaye anamiliki viwanda 41 alisema uamuzi aliochukua Rais Magufuli ni mzuri hasa katika kipindi hiki ambacho Tanzania inaelekea katika uchumi wa kati.

Dewji alisema kampuni yake ya MeTL Group itaendelea kushirikiana na serikali na katika kipindi cha miaka kadhaa ijayo amejipanga kuhakikisha anatoa ajira kwa Watanzania 100,000 jambo ambalo litasaidia kukuza uchumi wa nchi na kwa wananchi.

Dewji ambaye kwa mujibu wa jarida la Forbes ni tajiri namba moja nchini aliongeza kuwa utendaji wa Rais Magufuli ni wa kasi hivyo anategemea kuwa katika kipindi cha miaka michache ijayo uchumi wa Tanzania utakuwa umekuwa  sana.

Pia Dewji alizungumzia umuhimu wa mkutano wa GBF ambao umekutanisha watu kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika wakiwepo viongozi wa serikali za nchi za Afrika na wawekezaji alisema ni nafasi ya kipekee kwani pamoja na kujadili viwanda pia amepata nafasi ya kuwaelezea washiriki wa mkutano fursa za uwekezaji zilizopo hapa nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *