Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Daud Filex Ntibenda amewataka wakurugenzi wote wa mikoa mitatu ya kaskazini kubadilisha na kujenga mabanda mapya kwa ajili ya maonyesho ya nane nane yanayoendelea mkoani humo.
Mkuu wa mkoa huyo aliyasema hayo wakati akifungua maonyesho ya nane nane katika viwanja vya Themi nane nane jijini Njiro mkoani Arusha huku akiwataka Taso washirikiane na jiji na viongozi wa mikoa yote ili waweze kutengeneza ukumbi mkubwa wa kisasa.
Pia amesema kumekuwa na changamoto kwa wananchi kutoelewa kauli mbiu ya maonesho ya nane nane mwaka huu hivyo basi amewaagiza wakulima na wafugaji waweze kuingia katika mafunzo ya shamba darasa na kwenye mabanda ili waweze kupata elimu zaidi.
Vile vile Mkuu wa mkoa aliwaagiza washiriki wenye mabanda yenye teknolojia ya kilimo waandae taarifa fupi ambayo mwananchi atakwenda nayo nyumbani na zitakazowaletea mabadiliko katika maeneo wanayoyatoka.