Klabu ya Yanga inatarajia kesho kuelekea Singida kwa ajili ya mechi ya ligi kuu Tanzania Bara dhidi ya Singida United.
Kikosi hicho cha Yanga katika safari hiyo, kitaendelea kuikosa huduma ya wachezaji wake wa kigeni, Amissi Tambwe, Donald Ngoma na Thabani Kamusoko ambao bado hawajapona kwa asilimia 100.
Kocha wa timu hiyo, George Lwandamina amesema kuwa matokeo waliyoyapata dhidi ya Simba yamewapa ari ya kufanya vizuri kwenye mchezo wao huo wa ugenini.
Amesema tofauti kwao ni kwa kuwa wanacheza mchezo huo ugenini na Singida ni moja ya timu imara kwenye Ligi Kuu msimu huu.
“Naamini tutafanya vizuri, wachezaji wangu wana ari na morali ya juu hasa baada ya matokeo tuliyoyapata dhidi ya Simba… tumekuwa na wachezaji majeruhi ambao ni muhimu na mchango wao unahitajika, lakini tumefanikiwa kuhimili changamoto za Ligi Kuu,”.
Kikosi cha timu hiyo leo kitaanza mazoezi ya uwanjani kwenye uwanja wa Uhuru baada ya jana kufanya mazoezi ya viungo gym.
Yanga wataondoka Dar es Salaam leo kwa basi kuelekea Singida tayari kwa mchezo huo utakaopigwa Jumapili kwenye Uwanja wa Namfua ambao ukarabati wake umekamilika.
Mabingwa hao watetezi wanashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi wakiwa na pointi 16 sawa na vinara Simba, Mtibwa Sugar na Azam FC, lakini Wanamsimbazi hao wanabebwa na tofauti nzuri ya mabao ya kufunga na kufungwa.