Wakulima wawili wa Afrika Kusini waliomlazimisha mtu mweusi kuingia katika jeneza akiwa hai wamehukumiwa kifungo cha miaka 10 jela.
Theo Martins na Willem Oosthuizen walihukumiwa mnamo mwezi Agosti kwa jaribio la mauaji na utekaji nyara.
Walimtuhumu Victor Mlotshwa kwa kupita katika ardhi, wakamshambulia na kumlazimisha kuingia katika jeneza na kutishia kumchoma akiwa hai.
Kesi hiyo ilizua hisia nchini Afrika Kusini na kuangazia wasiwasi wa ubaguzi wa rangi katika jamii kadhaa za wakulima.
Bwana Mlotshwa aliripoti kisa hicho baada ya kanda ya video kuhusu unyanyasaji huo kutokea katika mtandao wa Youtube miezi kadhaa baadaye.
Katika hati ya kiapo mahakamani wawili hao walisema kuwa hawakuwa na lengo la kumuumiza bwana Mlotshwa wakati aliposhambuliwa mnamo mwezi Agosti 2016 na kwamba walitaka kumpatia funzo.
Haki miliki ya picha Reuters Image caption Victor Mlotshwa
Bwana Mlotshwa alikana kupita katika ardhi yao, akisema kuwa alikuwa akichukua njia ya mkato kwenda dukani ambapo alikuwa ametumwa na mamake.
Wakati wawili hao walipohukumiwa , jaji aliiambia mahakama ilikuwa wazi kwamba walilenga kumuua mwathiriwa.