Katibu mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa amewahimiza mashabiki wa timu hiyo kununua tiketi kwa wakati ili kuepuka usumbufu kutokana na idadi ndogo ya mashabiki wanaotakiwa kuingia uwanjani.
Akizungumza leo kwenye kikao na Wanahabari Mkwasa amesema ni vyema kila shabiki wa Yanga anayetaka kuingia uwanjani akanunua tiketi kwa muda uliopangwa.
“Ni vizuri mashabiki wetu wakanunua tiketi kwa muda uliopangwa kwani uwanja wa Uhuru ni mdogo ukilinganisha na uwanja wa taifa hivyo hata idadi ya mashabiki itakuwa ndogo, ila kwa wale watakaokosa tiketi ni vyema wakatafuta namna nyingine ya kutazama mchezo huo”, amesema Mkwasa.
Aidha Mkwasa amezungumzia pia ujenzi wa uwanja wa Kaunda uliopo makao makuu ya timu hiyo mitaa ya Jangwani ambapo amebainisha kuwa taratibu za ujenzi huo zinaendelea vizuri.
Wakati huohuo Makamu Mwenyekiti wa soka la Wanawake klabu ya Yanga Siza Lyimo, amesema usaili wa kutafuta wachezaji watakaounda timu itakayojulikana kama Yanga Princess unaanza leo mpaka October 31.