Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) limetangaza matokea ya mtihani wa darasa la saba huku ufaulu ukizidi kuongezeka.
Matokeo hayo yametangazwa leo na Katibu Mtendaji wa Necta, Dkt. Charles Msonde alipokuwa akitangaza matokeo hayo, ambapo amesema kuwa watahiniwa 662,035 kati ya 909,905 waliofanya mtihani huo wamefaulu kwa alama 100.
Amesema kuwa kati waliofaulu, wasichana ni 341,020 ambao ni sawa na asilimia 70.93 na wavulana ni 321,015 ambao ni sawa na asilimia 74.80, na kuongeza kuwa idadi ya watahiniwa waliofaulu ni sawa na asilimia 72.76.
Aidha, Dkt. Msonde amesema kuwa mwaka 2016 watahiniwa waliofaulu walikuwa asilimia 70.36 hivyo kuna ongezeko la ufaulu kwa asilimia 2.40.
Dkt. Msonde amezitaja shule zilizoshika nafasi kumi 10 bora za kitaifa kuwa ni, St. Peter (Kagera), St. Severine (Kagera), Alliance (Mwanza), Sir John (Tanga), Palikas (Shinyanga), Mwanga (Kagera), Hazina (Dar es salaam), Rweikiza (Kagera) Martine Luther (Dodoma) na St. Anne Marie iliyopo Dar es salaam.
Hata hivyo, pia amezitaja shule 10 ambazo hazikufanya vizuri kitaifa kuwa ni, Nyahaa (Singida), Bosha (Tanga) Ntalasha (Tabora), Kishangazi (Tanga), Mntamba (Singida), Ikolo (Singida), Kamwala (Songwe), Kibutuka (Lindi), Mkulumuzi (Tanga) na Kitwai A ya Manyara.
Vile vile, ameitaja mikoa iliyoongoza kitaifa kuwa Dar es salaam, Geita, Kagera, Iringa, Kilimanjaro, Njombe, Arusha Mwanza na Katavi.