Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari amesema kuwa hatokaa kimya endapo haoni hatua zinazochukuliwa kuhusu madiwani walioongwa.
Nassari amesema hayo leo baada ya Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Valentino Mlowola kumtaadharisha Nassari kuacha kugeuza taarifa anazoziwasilisha kwenye taasisi hiyo kuwa ni za kisiasa.
Awali akizungumza leo Jumanne asubuhi, Mlowola ametoa tahadhari hiyo kwa Nassari leo Jumanne, Oktoba 17, 2017 alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Amesema endapo Nassari ataendelea kuingiza siasa kwenye suala hilo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Mlowola amesema kitendo cha mwanasiasa huyo kuweka hadharani taarifa za uchunguzi ni kinyume cha sheria kwa kuwa kazi hiyo inatakiwa kufanyika kwa siri na Mahakama ndiyo yenye jukumu la kuchukua hatua.
Amesema Takukuru ina wajibu wa kumlinda mtoa taarifa lakini jukumu hilo linakuwa tofauti kwa Nassari ambaye ameamua kujitokeza hadharani.
Mkurugenzi mkuu huyo amemtaka Nassari kuacha kukiingiza chombo hicho kwenye siasa ili kifanye kazi kwa uhuru kama sheria inavyoelekeza.