Kocha wa Tottenham, Mauricio Pochettino amesema timu yake haijajiandaa kumkabili Ronaldo bali inakwenda kukabiliana na timu ya Real Madrid.
Pochettino ameyasema hayo leo wakati wakijiandaa na safari yao kuelekea nchini Hispania kwenye mchezo wa ligi ya mabingwa barani Ulaya UEFA siku ya kesho dhidi ya mabingwa watetezi Real Madrid.
Pochettino amesisitiza kuwa Tottenham ina iheshimu Real Madrid na kamwe hawezi kusema ni timu ya Ronaldo. Kauli hiyo ya Pochettino imeendelea kutafsiriwa kama mwendelezo wa majibizano yake na Pep Guardiola ambaye wikiendi iliyopita aliiita Tottenham kuwa ni timu ya Harry Kane kitendo ambacho kilimkera Pochettino.
Tottenham inakutana na Real Madrid kwenye mchezo wa tatu wa kundi H ambapo timu hizo zitakuwa zinagombania kuongoza kundi ikiwa tayari zote zina alama 6 baada ya kushinda mechi zao mbili za mwanzo.
Katika michezo mitano ambayo timu hizo zimekutana Real Madrid imeshinda mara tatu, zikitoka sare mara mbili.