Polisi nchini Kenya wametumia mabomu ya machozi kuwatawanya wafuasi wa muungano wa upinzani National Super Alliance waliokuwa wakiandamana katika miji mikubwa mitatu nchini humo.
Muungano huo umekuwa ukifanya maandamano kushinikiza mageuzi kwenye Tume ya taifa ya Uchaguzi IEBC kabla ya uchaguzi mpya kufanyika.
Mahakama ya Juu nchini humo ilifuta matokeo ya uchaguzi wa urais uliofanyika tarehe 8 Agosti ikisema ulijaa kasoro nyingi kiasi kwamba ilikuwa vigumu kubaini nani alishinda kwa njia halali.
Serikali ilipiga marufuku maandamano katika maeneo ya kati ya miji ya Nairobi, Mombasa na Kisumu baada ya visa vya uporaji kushuhudiwa wakati wa maandamano ya awali.
Jijini Nairobi, polisi wamekuwa wakishika doria katika barabara kuu kuwazuia waandamanaji kuingia katikati mwa jiji.