Mvua zinazoendelea kunyesha mkoani Tabora zimesababisha vifo vya watu watano katika maeneo tofauti tofauti wilayani Igunga mkoani humo..

Hayo yamesemwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora, Wilbroad Mtafungwa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, mbapo amewataka wananchi kuchukua tahadhari mapema.

Amesema kuwa katika tukio la kwanza mnamo tarehe 11 mwezi huu watu wanne wamefariki dunia baada ya kuangukiwa na ukuta wa nyumba waliyokuwa wakiishi kufuatia mvua zilizonyesha kwa kipindi cha siku mbili.

Aidha, Mtafungwa amesema kuwa waliofariki kwa kuangukiwa na ukuta wanatoka kijiji cha Igogo kata ya Nanga na kuwataja kuwa ni Kang’wa Makenza (80) ambaye pia ni mmiliki wa nyumba iliyosababisha maafa hayo, wengine ni Sande Dule (6), Butonda Shija(3) na Mbula Dule mwenye miezi miwili.

Hata hivyo, ameongeza kuwa Katika tukio la pili lililotokea katika kijiji cha Bulyang’ombe kata ya Nanga mtoto aliyejulikana kwa jina la Zenga Tano (5) alifariki dunia baada ya kupigwa na radi wakati amelala na wazazi wake.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Igunga, John Mwaipopo amewashauri wakazi wa Igunga kufuata utalaamu wa ujenzi wakati wa ujenzi wa nyumba zao ili kuepuka maafa zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *