Rais wa Nicaragua, Daniel Ortega amemtaja mkewe kama mgombea mwenza na makamu wa rais wakati huu ambapo anawania kuchaguliwa kwa muhula mwengine.
Mkewe Rosario Murillo tayari ana wadhfa maarufu wa msemaji wa serikali na anaonekana kuwa anagawana mamlaka na mumewe.
Wakosoaji wanawashtumu wanandoa hao wawili kwa kuiendesha Nicaragua ambayo inakabiliwa na uchaguzi mkuu mwezi Novemba kama chombo chao cha kibinafsi.
Rais Ortega akiwa hazungumzi sana katika vyombo vya habari ,mkewe huonekana mara kwa mara katika runinga akijadili sera na kujikuza .
Akiwa mama wa watoto 7 wa rais huyo anajua kuongea Kiingereza na Kifaransa huku akijulikana pia kuwa mshairi na pia anasifa za kuvaa mavazi yenye rangi nyingi na vito vya miaka ya sitini.
Wanahabari wamesema kuwa raia wengi wa taifa hilo wanamuona bi Murillo kama mwenye uwezo mkubwa katika taifa lake kutokana na hadhi yake katika uma.
Mume na mkewe waliwasilisha makaratasi yao ya kugombea viti hivyo rasmi katika mji mkuu wa Managua wakiandamana na mshauri wakili wa chama chao cha Sandinista.