Serikali ya China imeipatia Tanzania msaada wa Shilingi 29.4bilioni kwa ajili ya kusaidia sekta ya elimu, utalii wa kijiolojia na kuukarabati Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.
Makubaliano ya msaada huo yametiwa saini Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Doto James, kwa niaba ya Serikali, na Kaimu Balozi wa China hapa nchini, Gou Haodong.
Katibu huyo amesema 22.4bilioni zitatumika kujenga Chuo cha Ufundi Stadi-VETA wilayani Ngara mkoani Kagera.
Ameeleza kwamba kiasi hicho pia kitatumika kujenga majengo ya utawala, mabweni, nyumba za walimu na miundombinu mingine itakayosaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia kwenye chuo hicho.
Katibu Mkuu huyo amesema China, itatoa 6.7bilioni kwa ajili ya kuukarabati Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam.
Amesema kiasi kingine cha shilingi 300milioni zitatumika kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu wa kuanzishwa kwa aina mpya ya utalii ujulikanao kama utalii wa kijiolojia “Geopark Project” katika Hifadhi ya Taifa Ngorongoro, mkoani Arusha.
Alisema lengo la utafiti huo ni kuhakikisha kuwa Tanzania inanufaika na maajabu mbalimbali ya kitalii yaliyopo nchini ambayo hayajatumika kikamilifu kuvutia watalii watakaoongeza pato la Taifa
Tangu miaka ya 1960 mpaka sasa nchi hiyo imeendelea kuisaidia Serikali katika ujenzi wa miradi mbalimbali ukiwemo upanuzi wa Chuo cha Polisi Moshi, Ujenzi wa Maktaba mpya katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na ujenzi wa Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Kuhusu masuala ya utalii wa kijiolojia katika Hifadhi ya Taifa Ngorongoro, amesema Tanzania ina bahati ya kuwa na vivutio vingi vya utalii lakini haijavutia idadi kubwa ya watalii kutoka China kuja kuvitembelea.