Kampeni ya ukusanyaji wa damu salama inaanza leo ambayo itadumu kwa takribani siku tano mfululizo huku baadhi ya mikoa kadhaa ikitajwa kuendesha kwa kampeni hiyo katika maeneo mbali mbali ya nchi.
Afisa Uhusiano wa Mpango wa taifa wa damu salama, Rajab Mwenda ameeleza kuwa kampeni hii inayo anza leo inampango wa kukusanya damu chupa zipatazo 6000 ili kuweza kukabiliana na mahitaji ya damu katika vituo vya Afya.
Afisa habari huyo amezungumzia vigezo ambavyo mchangiaji anastahili awe navyo ambapo amesema kuwa mchangiaji wa damu inabidi awe na umri wa kuanzia miaka 18-65, awe na uzito wa kilo 50 awe na afya bora, pamoja na kuwa na wingi wa damu wa 85% na kuongeza kuwa mwanaume anauwezo wa kuchangia damu kila baada ya miezi 3 na mwanamke anauwezo wa kuchangia damu kila baada ya miezi 4.
Amefafanua sababu ambazo zinafanya mchangiaji awe hana sifa ya kuchangia damu ni pamoja na wanawake wajawazito ambao hawaruhusiwi kuchangia damu watu wote wenye shinikizo la damu pamoja na wenye tabia hatarishi.
Hata hivyo, Mwenda amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi katika wiki hii na kuwasisitizia kutoa taarifa kwa wauguzi wote ambao wamekuwa wakitaka pesa kwa ajiri ya kulipia damu.
Miongoni mwa mikoa ambayo itaendesha kampeni hizi ni pamoja na Kilimanjaro, Mtwara, Tabora, Mbeya, Mwanza pamoja na Dar es Salaam na mpango huo wa uchangiaji wa damu salama utakuwa unafanyika kila robo ya mwaka.