Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesikitishwa na  kitendo cha mwalimu wa Shule ya Msingi Samanzi, iliyoko kijiji cha Samanzi, Kata ya Kisumba, wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa kumpa ujauzito mwanafunzi wa darasa la saba.

Waziri Ummy amesema kitendo hicho ni ukatili na unyanyasaji dhidi ya mtoto wa kike na ni ukiukwaji wa Haki za Msingi za Mtoto ikiwemo haki ya Kuendelezwa na Kulindwa.

Waziri Ummy amewaasa walimu kuacha tabia ya kuwa na mahusiano ya kingono na wanafunzi maana shule kama taasisi, ni chombo madhubuti cha kujenga uelewa kwa jamii kuhusu ulinzi na usalama wa Mtoto katika jamii.

Pia Waziri amewataka walimu,  walezi na jamii kuhakikisha wajibu wa kuwalinda na kuwalea watoto bila uwanyanyasaji na ukatili wa aina yoyote.

Ameongeza kuwa, inapotokea mwalimu amehusishwa na tuhuma ya kumpa mimba mtoto wa kike kitendo hicho kinatia doa dhamana ya mwalimu na nafasi ya shule katika malezi ya mtoto.

Waziri Ummy, ameitaka jamii kuboresha ushirikiano wa wazazi, walezi na walimu maana wanamchango mkubwa katika makuzi na maendeleo ya watoto.

Waziri Ummy amesisitiza kutambua kuwa madhara ya mwalimu kumpa mimba mwanafunzi anamfanya kuwa mwathirika wa vitendo vya ukatili katika maisha yake yote.

Waziri Ummy ameelekeza vyombo vya dola mkoani Rukwa kuhakikisha suala hili linachunguzwa kikamilifu na kumfikisha mtuhumiwa mbele ya vyombo vya sheria ili haki iweze kutendeka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *