Idadi ya wakimbizi wa Sudani Kusin wanaoingia kwenye kambi nchini Uganda imeongezeka maradufu ndani ya kipindi cha siku 10 tu.
Shirika la Umoja wa mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limesema kuwa zaidi ya wakimbizi 60,000 wamevuka mpaka wa Sudani Kusini na kukimbilia kwenye nchi za Uganda, Kenya na Sudan.
Miongoni mwa wakimbizi hao 52,000 wamevuka mpaka na kuingia Uganda baada ya mapigano kuzuka huku wakimbizi zaidi ya 7,000 wakikimbilia Sudani Kaskazini na 1,000 wakiingia Kenya.
Wakimbizi hao wamekimbia mapigano yaliyozuka upya nchini juba kati ya vikosi tiifu kwa serikali ya Salva Kiir na wapiganaji wanaomuunga mkono aliyekuwa makamu wa rais Riek Machar.
Wakati huo huo, kuna taarifa kuwa makundi ya watu wenye silaha yamekuwa yakipita barabarani na kuzuia wakimbizi hao kuvuka mpaka kuingia Uganda.
Wakimbizi wanaotokea kwenye mkoa wa Yei, wamedai kuwa walipokea barua iliyowatahadharisha kuhama eneo hilo kutokana na mapigano baina ya serikali na waasi.