Mbunge wa umri mdogo zaidi nchini Kenya amekabidhiwa gari ambalo alikuwa ameahidiwa na Rais Uhuru Kenyatta.

John Paul Mwirigi, 23, ambaye ni mbunge wa Igembe Kusini, takriban kilomita 200 mashariki mwa jiji la Nairobi, alichaguliwa akiwa bado mwanafunzi wa chuo kikuu.

Bw Mwirigi alitumia baiskeli na pikipiki za kusafirisha abiria, maarufu kama bodaboda, kuwafikia watu wakati wa kampeni.

Wakati wa kuapishwa, alitumia magari ya uchukuzi wa umma, kufika majengo ya Bunge jijini Nairobi.

Wabunge walipoalikwa ikulu, alipewa lifti na mbunge mwenzake mpaka kufika eneo hilo kutokana na kukosa gari.

Hata hivyo, wakati wa kuondoka, alitumia gari la abiria maarufu kama matatu nchini Kenya kwa kuwa hana gari.

John Paul Mwirigi ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu Somo la Ualimu katika Chuo Kikuu cha Mt Kenya alitangazwa mshindi baada ya kupata kura 18,867 na kumshinda mpinzani wake wa karibu Rufus Miriti wa chama cha Jubilee chake Rais Kenyatta, ambaye alikuwa na kura 15,411.

Wagombea wengine, ambao wamekuwa wanasiasa kwa muda mrefu walikuwa ni Mwenda Mzalendo aliyepata kura 7,695, Kubai Mutuma (6,331) na Raphael Muriungi (2,278).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *