Jeshi la Polisi nchini limewataka watu mbalimbali akiwemo Mbunge Halima Mdee, walioripoti kwenye mitandao ya kijamii na kusambaza picha ya askari wake akihusishwa na tukio la Tundu Lissu kuripoti kwa DCI kwa ajili ya mahojiano zaidi.
Taarifa hiyo imetolewa leo na msemaji wa Jeshi la Polisi nchini ACP Barnabas David kwenye mkutano wake na waandishi wa habari, na kuwataka watu hao akiwemo mbunge huyo wa Kawe kwa tiketi ya CHADEMA kujisalimisha wenyewe kwa kutoa taarifa za uongo.
Pia amesema kwamba jeshi la polisi kitengo cha upelelezi wa makosa ya mtandaoni kinaendelea na uchunguzi, kuwabaini wote waliohusika na kusambaza kwa taarifa hizo za uongo ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.