Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro amesema watu ambao wamefanya uhalifu wa kumpiga risasi Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu kuwa wanaweza kupatikana ikiwa wananchi watasaidia jeshi hilo kupata taarifa za wahalifu hao.
Sirro amesema hayo leo alipokutana na waandishi wa habari akielezea hali ya usalama wa nchi na kudai usalama wa nchi upo vizuri na kuwa mpaka sasa jeshi la polisi limeongeza nguvu ya upelelezi mjini Dodoma ili kuhakikisha linawapata watu ambao wamefanya uhalifu wa kumpiga risasi mbunge Tundu Lissu , huku akiwataka wananchi wasihusishe tukio hilo na masuala ya kisiasa.
IGP Sirro amezungumzia kuhusu moja ya kauli ya Tundu Lissu ambayo aliwahi kusema kuwa kuna watu wanamfuatilia na kuvitaka vyombo vya usalama kuacha kuwatuma watu hao kumfuatilia na kudai kuwa hakuwahi kuripoti katika kituo chochote cha polisi, na kusema sasa usiwe wakati wa kuzungumzia jambo hilo.
IGP Sirro alimalizia kwa kusema kuwa jeshi la polisi lipo imara na lipo kwa ajili ya kulinda watanzania pamoja na mali zao na si kuwaumiza watanzania hivyo ametoa rai kwa wananchi kushirikiana na jeshi la polisi kuwapata watuhumiwa hao.