Kiongozi wa upinzani nchini Togo amemtaka Rais Faure Gnassingbe ambaye yeye na familia yake wameiongoza nchi hiyo kwa miaka hamsini kujiuzulu mara moja akipinga hatua ya serikali ya kutaka kuibadilisha katiba.

Maelfu ya waandamanaji walimiminika katika barabara za mji mkuu wa Togo, Lome wakiwa wamevalia nguo za rangi za nyekundu, chungwa na waridi, rangi za vyama vya upinzani huku maafisa wa usalama wakiwatizama.

Mkuu wa shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International nchini humo Aime Adi amesema zaidi ya waandamanaji laki moja walishiriki maandamano hayo ya kuishinikiza serikali kutobadilisha katiba kwa njama ya kusalia madarakani.

Rais Gnassingbe ameliongoza taifa hilo la Afrika magharibi tangu baba yake afariki mwaka 2005 baada ya kuwa madarakani kwa miaka 38.

Gnassingbe Eyadema alipitisha sheria mwaka 1992 ya kuwa mihula ya kuhudumu kwa rais ni miwili pekee lakini muongo mmoja baadaye aliifutilia mbali sheria hiyo.

Baraza la mawaziri siku ya Jumanne lilidhinisha mswada wa kurejesha kikomo cha mihula ya rais lakini uamuzi huo wa baraza la mawaziri haukutuliza upinzani ambao umenoa makali.

Akizungumza mbele ya umati mkubwa wa waandamanaji hao mjini Lome, Jean Pierre Fabre kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha ANC amesema wataandamana tena leo na Rais lazima awazungumzie kuhusu namna ya kuondoka madarakani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *