Rais wa awamu ya nne wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amevitaka vyama tawala barani Afrika kutowachukulia viongozi wa upinzani kuwa maadui na badala yake kuwafanya kuwa washirika wakuu umeungwa mkono na wengi.
Akizungumza katika mkutano wa viongozi wa Afrika Kuhusu uongozi bora na sheria uliofanyika mjini Johannesburg, Kikwete alitoa changamoto kwa vyama vya kisiasa barani Afrika kushirikiana.
Kikwete amesema badala ya kuuchukulia upinzani kuwa adui, wanafaa kuchukuliwa kuwa washirika katika kuimarisha demokrasia inayoheshimu sheria.
Kufuatia taarifa hiyo mchanganuzi wa maswala ya kisiasa kutoka chuo kikuu cha kikatholiki cha Ruaha Prof Gaudence Mpangala alinukuliwa na gazeti la The Citizen nchini Tanzania akisema kuwa taarifa hiyo ya rais Kikwete inafaa kupongezwa.
Bwana Mpangala amesema kuwa ni muhimu kwamba taarifa hiyo inatoka kwa kiongozi mwandamizi katika chama cha CCM.
Kuendelea kuwanyima wapinzani haki ya kutekeleza wajibu wao ni sawa na kuwanyima raia haki zao kimaendeleo.
Kwa mujibu wa gazeti hilo bwana Mpangala amesema kuwa matatizo mengi yanayokabili Afrika yanatokana na ukandamizaji wa sera za kidemokrasia.