Mahakama ya Juu nchini Kenya imeukubalia muungano wa upinzani nchini humo National Super Alliance (Nasa) kupekua mitambo iliyotumiwa na tume ya uchaguzi nchini humo wakati wa uchaguzi uliofanyika tarehe 8 Agosti.
Mahakama hiyo imesema muungano huo utaweza kusoma data kwenye sava hizo chini ya uangalizi kuhakikisha usalama wa mitambo ya IEBC hauhujumiwi.
Mgombea wa Nasa Raila Odinga amewasilisha kesi mahakamani kupinga ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta wa chama cha Jubilee.
Mawakili wa Bw Odinga wameruhusiwa na mahakama kunakili data kutoka kwenye sava hizo kwa ajili ya kufanya uchunguzi kuhusu uchaguzi huo.
Miongoni mwa mengine, upinzani utapata utambulisho wa sava zilizotumiwa wakati wa uchaguzi, ukuta wa kinga uliotumiwa kulinda sava hizo pamoja na mitambo ya dijitali ya uchaguzi wa Kenya (KIEMS) dhidi ya wadukuzi na mfumo endeshi wa mitambo hiyo pamoja na nywila zilizotumiwa kuingia katika mitambo hiyo.
Kadhalika, wataweza kupata taarifa kuhusu yaliyojiri katika mitambo hiyo ya uchaguzi kuanzia Agosti tano hadi leo.
Aidha, wataruhusiwa kusoma nakala za Fomu 34A na 34B (fomu za matokeo katika vituo vya kupigia kura na ngazi ya maeneo bunge) ambazo zilitumiwa kutangaza matokeo.
Taarifa kuhusu mchakato wa upinzani kupekua sava na mitambo hiyo ya IEBC itawasilishwa kwa mahakama hiyo kesho jioni.
Majaji saba wa mahakama hiyo ya juu wameanza kusikiliza kesi hiyo iliyowasilishwa na Bw Odinga leo.
Kwa mujibu wa matokeo ya IEBC, Rais Kenyatta alipata kura 8,203,290 huku naye Raila Odinga akipata kura 6,762,224.