Baraza la Vijana Chadema wamelitaka jeshi la polisi nchini kumkamata, William Ngeleja kwa kukutwa na mali ya wizi kutoka (Escrow) na kumuachia Tundu Lissu kwa kusaidia kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu ndege ya Tanzania kukamatwa huko nchini Canada.

Akisoma barua aliyoiandika kwenda kwa Mkuu wa Jeshi la polisi nchini Simon Sirro, na Mkurugenzi wa makosa ya upelelezi mbele ya wanahabari  mapema leo jijini Dar es salaam, Mwenyekiti wa BAVICHA, Patrobas Katambi amesema aliyekuwa Waziri wa Nishati na Mdini, Mh. William Ngeleja kupitia pesa alizozirudisha hivi karibuni ni wazi kuwa ni mtuhumiwa ambaye anaweza kutaja wenzake wote kisha wakarudish bilioni 307 ambazo zilichotwa kutoka akaunti ya Tegeta Escrow.

Katambi amesisitiza kwamba hakuna haja ya kumshikilia Lissu pasipokuwa na sababu za msingi kutokana na mamlaka waliyonayo bali wanapaswa kuhakikisha wanawaweka ndani watuhumiwa waliosababishia serikali hasara ya mabilioni ikiwepo kampuni ya Lugumi pamoja na watu waliogawana pesa za Escrow.
Pamoja na hayo Mwenyekiti huyo ambaye ni Mwanasheria kitaaluma ameongeza kuwa iwapo jeshi la polisi litashindwa kuwatia nguvuni  Ngeleja na wenzake wao wenyewe watafanya kazi hiyo kwa kutumia sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai ya 2002 ijulikanayo kama “Arrest by private person’.

Aidha Katambi amesema kuwa kupitia barua hiyo wasipopata majibu  yao watafanya maandamano ya amani nchi nzima ili kuweza kushinikiza haki za kisheria, kiuchumi na kisiasa nazo zifuatwe huku wakiwafundisha vijana namna ya kudai haki zao za msingi.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *