Zaidi ya nyumba 286 zilizopo Kimara Stop Over zilizowekewa kinga ya muda na Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi zimebomolewa.

Hiyo ni sehemu ya operesheni ya kubomoa nyumba zaidi ya 1,300 zilizo ndani ya hifadhi ya Barabara ya Morogoro kuanzia Kimara hadi Kiluvya.

Wakati kazi ya kubomoa nyumba hizo ikiendelea, diwani wa zamani wa Saranga, Ephrahim Kinyafu alisema kinga ya muda kuzuia nyumba kubomolewa ilitolewa Agosti 18 baada ya wananchi 286 kwenda mahakamani na kwamba wamesikitishwa kuona zinabomolewa licha ya hati ya kuzuia kutolewa.

Kinyafu alisema walikwenda mahakamani kwa kuwa ndicho chombo chenye mamlaka ya kusimamia sheria.

Mbunge wa Kibamba, John Mnyika alisema uamuzi huo ni kinyume cha sheria na ameitaka Mahakama kuingilia kati na kuchukua hatua dhidi ya Tanroads.

Mhandisi wa wakala huyo Kimara, Johnson Rutechura alisema, “Hatuna taarifa juu ya nyumba ambazo zina kinga.”

Msimamizi huyo wa bomoabomoa alisema hawakupewa barua yoyote kutoka mahakamani hivyo hawatambui kama kuna nyumba zenye zuio.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *