Muungano wa upinzani nchini Kenya, National Super Alliance (NASA) umewasilisha kesi ya kupinga ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 8 Agosti.

Mawakili wa muungano huo wamewasilisha nyaraka za kesi hiyo na ushahidi katika majengo ya Mahakama ya Juu mjini Nairobi takriban saa moja unusu kabla ya muda ulioruhusiwa kumalizika.

Nyaraka na stakabadhi za ushahidi zilizowasilishwa na muungano huo ni za kurasa 9,000 zilizokuwa kwenye uchaguzi huo.

Kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais yaliyotangazwa Ijumaa wiki iliyopita ilifaa kuwasilishwa kabla ya saa sita usiku leo, kabla ya kumalizika kwa siku saba tangu kutangazwa kwa matokeo.

Mgombea urais wa chama hicho waziri mkuu wa zamani Raila Odinga alikuwa ameapa kutopinga matokeo ya urais tena kortini kabla ya uchaguzi kufanyika na baada ya matokeo kutangazwa.

Lakini alibadilisha uamuzi huo na kutangazwa Jumatano wiki hii kwamba muungano wake ungefika kortini kupinga matokeo hayo.

Bw Odinga alisema ingawa muungano huo ulikuwa umeapa kutowasilisha kesi kortini wakati huu, waliona ni heri kufanya hivyo “kufichua uovu uliotokea wakati wa uchaguzi mkuu.”

Bw Odinga alisema mitambo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi IEBC ilidukuliwa na matokeo kuvurugwa kumfaa Bw Kenyatta ambapo kulikuwa na pengo kiasi fulani kati yake yeye na Bw Kenyatta muda wote wa kutangazwa kwa matokeo.

Aidha, kiongozi huyo aliishutumu tume ya uchaguzi akisema ilikuwa ikitangaza matokeo ya uchaguzi bila kutoa Fomu 34A za kuonyesha matokeo yalivyokuwa katika vituo vya kupigia kura.

Jamii ya kimataifa ilikuwa imehimiza upinzani, pamoja na wagombea wengine ambao hawakuwa wameridhishwa na uchaguzi, kutumia mifumo iliyowekwa kikatiba kutafuta haki.

Kwa mujibu wa matokeo ya IEBC, Rais Kenyatta alipata kura 8,203,290 huku naye Raila Odinga akipata kura 6,762,224.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *