Baada ya kukaa jela kwa miezi mitano, hatimaye kiongozi mkuu wa upinzani nchini Zambia, Hakainde Hichilema ameachiwa huru.
Kiongozi huyo ameachiwa huru baada ya Mwendesha Mashtaka kumfutia mashtaka kiongozi huyo aliyekuwa mahabusu tangu Aprili mwaka huu.
Hichilema na wenzake walikamatwa kwa madai ya kutaka kuhatarisha maisha ya Rais wa Zambia, Edgar Lungu baada ya kiongozi huyo na wafuasi wake kukataa kupisha msafara wa rais huyo.
Habari za kuachiwa huru zilivuja tangu mwishoni mwa wiki, ikielezwa kwamba ni kutokana na juhudi zilizofanywa na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Patricia Scotland ambaye alifanya ziara nchini Zambia kuangalia hali ya siasa.
Katibu huyo alikutana na kufanya mazungumzo na Rais Lungu na pia alimtembelea Hichilema katika gereza la Mukobeko.