Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limeanza kutekeleza operesheni iliyoitangaza wiki iliyopita kwa kuwaondoa wapigadebe kwenye vituo vya daladala kutokana na kuwa chanzo cha wizi.

Kaimu Kamanda wa Kanda Maalum Dar es Salaam, Lucas Mkondya,  jana alisema kuwa, operesheni hiyo imeanza jijini baada ya kukithiri kwa kesi zitokanazo na wizi kwenye vituo hivyo.

Alisema kwa siku kunaripotiwa matukio 20 hadi 50 ya wizi kwenye vituo vya daladala jijini huku wapigadebe wakidaiwa kuwa kichaka cha wizi huo.

Alisema operesheni hiyo, itakayoendeshwa kwa wiki nzima imelenga kuvifanya vituo hivyo kuwa maeneo salama.

Agizo la Kamanda Mkondya si jipya hata hivyo kwa wapiga debe baada ya maazimio kama hayo, kadhaa kushindwa katika miaka ya nyuma.

Akizungumza Machi 16, mwaka jana jijini, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawane alimtaka Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuhakikisha anawaondoa wapiga debe wote kwenye vituo vya mabasi kwa sababu hizo hizo.

Waziri Simbachawene alitoa agizo hilo, wakati wa semina kwa wakuu wa mikoa wote nchini ambao walikuwa wameapishwa na Rais John Magufuli, Ikulu katika siku iliyotangulia.

Waziri huyo, alisema kazi ya kupiga debe sio rasmi na isiyo na kipato kitachoweza kumkwamua kijana husika kuondokana na umaskini.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *