Kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga amewashauri wafuasi wake kususia kazi kama njia ya kupinga matokeo ya uchaguzi uliofanyika Jumanne iliyopita.

Akihutubia wafuasi wake mtaani Kibera, Nairobi kwa mara ya kwanza kabisa tangu kutangazwa matokeo, ambapo Rais Uhuru Kenyatta alitangazwa mshindi, Odinga amedai kuwa serikali ilikiwa imepanga kuwaua wafuasi wa upinzani kabla ya kutangazwa matokeo.

Hii ni siku moja baada wa watu kadha kuripotiwa kuuawa maeneo tofauti ya mji wa Nairobi na Kisumu, wakati wafuasi wa upinzani walijitokeza kulalamikia matokeo ya uchaguzi

Aidha Odinga amesema kuwa siku ya Jumanne, mrengo wa Nasa utatangaza mwelekeo ambao utachukua.

Bw Odinga baadaye alizuru mtaa wa Mathare Kaskazini jijini Nairobi ambapo msichana wa miaka tisa alifariki baada ya kupigwa risasi wakati wa makabiliano kati ya polisi na waandamanaji.

Rais Uhuru Kenyatta alitangazwa mashindi kwa kura 8,203,290 huku naye Raia Odinga akipata kura 6,762,224.

Katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan, ambaye alikuwa mpatanishi mkuu baada ya mzozo wa kisiasa nchini Kenya miaka kumi iliyopita, alikuwa ametoa wito kwa Bw Odinga kutumia mifumo ya kisheria kutafuta haki kuhusu matokeo ya uchaguzi wa urais.

Annan alikuwa mpatanishi mkuu baada ya ghasia kuzuka baada ya uchaguzi mkuu wa 2007 uliokumbwa na utata.

Mwaka 2007, watu zaidi ya 1,000 walifariki na wengine 600,000 wakafurushwa makwao wakati wa ghasia za kikabila zilizozuka baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *