Aliyekuwa mgombea urais wa Kenya anayeungwa mkono na umoja wa NASA, Raila Odinga amehudhuria tukio la utangazaji wa matokeo Bomas jijini Nairobi licha ya kuyakataa matokeo yanayopeperushwa na Tume Huru ya Uchaguzi (IEBC).
Raila ameingia katika eneo hilo akiwa na kitendawili ambacho huenda akakitegua au la kwani ameendelea kushikilia msimamo wake kuwa matokeo yanayotolewa na IEBC yamechakachuliwa huku akitaka atangazwe kuwa mshindi.
Kambi ya NASA imedai kuwa kuna watu walidukua mfumo wa kutunza kumbukumbu wa IEBC na kugeuza matokeo na kwamba wana vielelezo vyote vinavyoonesha jinsi udukuaji huo ulivyofanyika.
NASA wamedai kuwa kwa mahesabu ya kura walizopata majimboni, Raila anaongoza akiwa na kura zaidi ya milioni nane, tofauti na kile kinachooneshwa na IEBC kuwa ana kura zaidi ya milioni 6 akiwa nyuma ya Rais Uhuru Kenyatta mwenye kura zaidi ya milioni nane.
Hata hivyo, IEBC wamekanusha madai yote ya kupinga matokeo yaliyotolewa na Raila na kambi ya NASA wakisisitiza kuwa kinachoonekana ndio uhalisia wa kilichotokea.
Kwa mujibu wa matokeo ya awali yaliyotolewa, Kenyatta anaonekana kuwa na kura 8,182,304 sawa na asilimia 54.22, na Raila ana kura 6,775,331 sawa na asilimia 44.89 ya kura zilizohesabiwa na kukubaliwa.