Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ameziagiza wizara za Fedha na Mipango na Tamisemi kuandaa mapendekezo na kupeleka bungeni mwaka huu marekebisho ya sheria yanayotaka kulipwa kwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa miradi inayopata ufadhili kutoka kwa wadau wa maendeleo ikiwemo Benki ya Dunia.
Alitoa agizo hilo juzi wakati akihutubia wananchi wa Korogwe waliohudhuria ufunguzi wa stendi mpya ya kisasa ya mabasi iliyogharibu Sh bilioni nne eneo la Kilole. Dk Magufuli alisema utaratibu huo unafanya serikali kulipa VAT kwa serikali yenyewe jambo ambalo si sahihi kwa kuwa fedha hizo zingetumika kufanya shughuli nyingine za maendeleo.
Alitoa agizo hilo baada ya Naibu Waziri Tamisemi, Selemani Jaffo kueleza kuwa ipo changamoto ya kisheria inayokabili miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali kutakiwa kulipa VAT na kusababisha serikali kulipa fedha za ziada Mamlaka ya Mapato (TRA) kwa sababu mikopo na ruzuku kutoka kwa wafadhili hazitengi malipo ya kodi.
Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba alimuomba rais kushughulikia mgogoro wa kiwanda cha kusindika chai cha Mponde wilayani Lushoto ambao umechukua muda mrefu na kusababisha wakulima wa Jimbo la Bumbuli wilayani humo kushindwa kujiendeleza kiuchumi.