Korea Kaskazini imesema kuwa inatafakari uwezekano wa kurusha makombora karibu na jimbo la Marekani la Guam katika bahari ya Pasifiki baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kuitishia Pyongyang kwamba itakabiliwa kwa moto na ghadhabu.

Shirika la habari la serikali ya Korea Kaskazini limesema taifa hilo linatafakari mpango wa kurusha makombora ya masafa ya kati na mbali karibu na Guam, eneo ambalo Marekani huwa na ndege zake za kuangusha mabomu.

Rais Trump ametoa tamko lake baada ya ripoti kwenye vyombo vya habari kusema kwamba Korea Kaskazini imeweza kuunda kichwa cha silaha za nyuklia chenye uwezo wa kutosha kwenye makombora yake.

Ufanisi huo, ingawa haujathibitishwa rasmi, ulitazamwa na wengi kama kiunzi cha mwisho kilichoizuia Korea Kaskazini kuwa taifa kamili lenye nguvu za silaha za nyuklia.

Taarifa ya gazeti la Washington Post, ikunukuu maafisa wa ujasusi wa Marekani, imedokeza kwamba Korea Kaskazini inaunda silaha za nyuklia zenye uwezo wa kuishambulia Marekani kwa kasi zaidi ya iliyotarajiwa.

Shirika la habari la Korea Kaskazini (KCNA) limesema jeshi la nchi hiyo “linachunguza kwa makini mpango wa kuanzisha moto wa kuzingira Guam kwa kutumia makombora ya roketi ya masafa ya wastani na ya masafa marefu ya Hwasong-12”.

Majibizano kati ya Marekani na Korea Kaskazini yamezidi baada ya Pyongyang kufanyia majaribio makombora mawili yenye uwezo wa kusafiri kutoka bara moja hadi nyingine, na kudai kwamba sasa ina makombora yanayoweza kufika Marekani bara.

Korea Kaskazini ilikuwa imeghadhabishwa na vikwazo vipya ilivyowekewa na Umoja wa Mataifa siku ya Jumamosi.

Vikwazo hivyo vina lengo la kupunguza mapato kutoka kwa mauzo ya bidhaa nje ya Korea Kaskazini kwa theluthi moja.

KCNA imesema Korea Kaskazini, ambayo imefanyia majaribio silaha za nyuklia mara tano, itajibu vikali na kwamba “Marekani italipia” kwa kuchangia kutunga vikwazo hivyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *