Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Edward Lowassa amefunguka sababu kuu zinazofanya amtetee na kumnadi mgombea Urais kupitia chama cha Jubilee Uhuru Kenyatta kuwa ni kiongozi shupavu.
Lowassa ambaye jana alishiriki katika mkutano wa chama cha Jubilee alisema kuwa kuna watu wanauliza kwanini yeye pamoja na CHADEMA wanamnadi kwa kuwa kiongozi huyo ni shupavu na mpenda watu.
“Kuna watu wananiuliza kwanini mnamnadi Uhuru Kenyatta, nasema tena hadharani bila aibu yoyote huyu ni kiongozi shupavu anayependa watu, anaweza kuongoza watu wetu, lakini cha pili Uhuru Kenyatta anapenda Afrika Mashariki akiingia madarakani ataturuhusu tuendelee kuzunguka zunguka kwenye mipaka hii kama Namanga pale bila hata shida, la tatu ni kwamba aliingia madarakani nchi ikiwa kwenye vita lakini amewapa suluhu ameingoza nchi imekwenda taratibu na akafanikiwa”.
Mbali na hilo Lowassa alisema kuwa licha ya mambo yote hayo lakini bado ukweli utabaki palepale kuwa Uhuru Kenyatta anapenda Demokrasia
“Tangu Demokrasia ya vyama vingi Uhuru Kenyatta hajaleta shida ya aina yoyote, siku moja nimeona kwenye TV yenu mama mmoja amemtukana mpaka matusi ya nguoni lakini asubuhi Rais anasema nimemsamehe bure, nawaambia huyu ndiye anawafaa, naondoka nikiwa na matumaini”.
Siku ya Jumanne Agosti 8 mwaka huu wananchi wa Kenya watakuwa wakifanya uchaguzi kuchagua viongozi wao mbalimbali.