Mbunge wa Mbozi (Chadema) Pascal Haonga ameendelea kushikiliwa na jeshi la polisi mkoani Songwe kwa kosa la uchochezi.
Hayo yamethibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Mathias Nyange huku akisema kuwa wanatarajia kumfikisha mahakamani baada ya kukamilisha upelelezi.
Kamanda Nyange amesema sababu za kumtia mbaroni Haonga ni kutokana na kufanya mkutano bila kibali cha polisi katika mji mdogo wa Mlowo-Mbozi na kuwahamasisha wamiliki wa malori na abiria kuandamana kwenda ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo Chiku Galawa.
Kamanda huyo amesema kuwa Haonga alifanya mkutano huo jana na alihamasisha madereva wa malori, wamiliki na abiria waende kumuona mkuu wa mkoa.
Kamanda ameendelea kusema kuwa lengo la mbunge huyo kuwataka watu hao wamuone mkuu wa mkoa ni kueleza kero yao juu ya adha ya usafiri baada polisi kupitia kitengo cha usalama barabarani kupiga marufuku malori kubeba abiria kutoka katikati ya mji wa Mlowo kwenda maeneo tofauti ya vijijini ambako hakuna usafiri mbadala zaidi ya malori.