Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amesema kuwa atakubali matokeo ya uchaguzi iwapo atashindwa kwa haki.
Rais Kenyatta ametoa hakikisho hilo wakati akijibu maswali mbalimbali kupitia runinga na kumtaka mpinzani wake Raila Odinga, naye kuwa tayari kufanya hivyo ikiwa atashindwa katika Uchaguzi huo.
Kenyatta amesema kuwa yeye ni mtu anayeheshimu uamuzi wa wananchi na kuwaomba wapinzani wake nao wafanye hivyo.
Amesema serikali yake imelenga Uchaguzi huo uwe wa amani ndiyo maana maafisa wa usalama wamejihami na wako tayari kukabiliana na wale watakaotaka kuzua fujo.
Naye Bw. Odinga, anayepeperusha bendera ya muungano wa upinzani NASA, amekuwa akisema kuwa atakubali matokeo hayo ikiwa Uchaguzi huo utakuwa huru na haki.
Hata hivyo, hivi karibuni ametoa madai mazito kuwa Rais Kenyatta anatumia jeshi kumsaidia kuiba kura, madai ambayo serikali imekanusha.