Vikosi maalumu vya majeshi ya nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) vimepiga kambi kwenye eneo la mapango ya Amboni, Tanga kwa ajili ya mazoez ya kijeshi.

Katika mapango hayo, mwaka jana yalitokea mauaji yaliyofanywa na watu wasiojulikana na kuzua hofu kwa wakazi wa eneo hilo ambao mwishowe walihamishwa na Serikali.

Akizungumza na waandishi wa habari   jana, Mkuu wa mpango huo, Meja Jenerali Harrison Msebo, alisema vikosi hivyo vitakuwa vikifanya mazoezi katika eneo hilo kama sehemu ya kupambana na ugaidi na uharamia baharini.

Kwa mujibu wa Meja Jenerali Msebo, mazoezi hayo yajulikanayo kwa jina la EX Matumbawe, yanatarajia kuanza Agosti 2 hadi Septemba mosi mwaka huu.

Alizitaja nchi zenye majeshi yatakayoshiriki mazoezi hayo  kuwa ni Afrika Kusini, Botswana, Lesotho, Malawi, Zambia, Zimbabwe   na wenyeji Tanzania.

Naye  Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela, alisema mazoezi hayo yataimarisha uhusiano wa kijeshi baina ya nchi wanachama wa SADC na yatawasaidia wanajeshi hao kubadilishana uzoefu katika utendaji kazi wao.

Wakati mazoezi hayo yakitarajia kuanza mwaka jana hali ilikuwa tete na ilizua taharuki jijini Tanga baada ya watu wasiojulikana, kuua idadi kadhaa ya watu katika eneo la mapango hayo.

Serikali ililazimika kupeleka vikosi vya Jeshi la Polisi na askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kwa ajili ya kukabiliana na wahalifu hao.

Wakati vikosi hivyo vya ulinzi na usalama vikifanya kazi, vilikuwa vikiendesha operesheni maalumu ya upekuzi ndani ya mapango hayo kwa lengo la kukabiliana na wahalifu hao.

Kutokana na hali ya usalama kuwa tete katika eneo hilo, baadhi ya watu walilazimika kuhama makazi yao kuokoa maisha yao.

 

 

 

.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *