Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo imemwachia kwa dhamana Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) na Rais wa Chama cha Wanasheria nchini, Tundu Lissu.
Lissu ametakiwa kudhaminiwa na wadhamini wawili ambao kila mmoja ataweka bondi ya dhamana ya shilingi milioni 10 huku akiwekewa zuio la kutoka nje ya Mkoa wa Dar es Salaam bila kibali maalum cha mahakama.
Tundu Lissu ambaye ni mwanasheria wa Chadema anadaiwa kutoa maneno ya uchochezi Julai 17, 2017 maeneo ya Ufipa Dar es Salaam.
Tundu Lissu alifikishwa Mahakamani leo baada ya kushikiliwa na Polisi akiwa Airport Dar es Salaam akielekea Kigali Rwanda kwenye Mkutano wa Mawakili.
Kesi yake imepangwa kusikilizwa Agosti 24 mwaka huu baada ya wadhamini wake kukamilisha taratibu zote za kumdhamini.