Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli jana ameweka jiwe la msingi la mradi wa maji wa Nguruka uliopo katika Wilaya ya Uvinza Mkoani Kigoma na kufungua miradi miwili ya barabara za Kaliua – Kazilambwa na barabara ya Tabora – Ndono – Urambo.
Mradi wa Maji wa Nguruka ambao utakamilika tarehe 31 Desemba, 2017 utagharimu Shilingi Bilioni 2.87 na ni miongoni mwa miradi 1,810 ya maji inayotekelezwa na Serikali kwa kutumia fedha za mfuko wa maji nchi nzima ambapo mpaka sasa miradi 1,333 kati yake imekamilika na miradi 477 ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Barabara ya Kaliua – Kazilambwa ina urefu wa kilometa 56 imejengwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 61.86 na barabara ya Tabora – Ndono – Urambo yenye urefu wa kilometa 94 imejengwa gharama ya Shilingi Bilioni 118.96, fedha za miradi yote miwili zimetolewa na Serikali ya Tanzania.
Akizungumza na wananchi katika sherehe za miradi hiyo pamoja na wananchi waliokuwa wakisimamisha msafara wake katika vijiji vya Uvinza, Mpeta, Usinge, Isawima, Igagala, Ndono, Kalola na Ilolangulu, Mhe. Rais Magufuli aliyeongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli alimuagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa kuhakikisha barabara za Urambo – Kaliua yenye urefu wa kilometa 28 inaanza kujengwa ndani ya mwezi mmoja na barabara ya Nyahua – Chaya yenye urefu wa kilometa 85 inaanza kujengwa ndani ya mwezi mmoja na nusu kwa kiwango cha lami.
Mhe. Rais Magufuli pia amewahakikishia wananchi wa Uvinza kuwa Serikali imeshapata fedha za kujenga barabara ya Uvinza – Malagarasi yenye urefu wa kilometa 50 na amemuagiza Waziri Mbarawa kuanza maandalizi ya ujenzi wa barabara ya Kazilambwa – Chagu yenye urefu wa kilometa 41.
Mhe. Rais Magufuli alisema Serikali imeweza kutekeleza miradi hiyo kwa fedha zake inazozipata kutokana na makusanyo ya kodi hivyo amewataka Watanzania kuhakikisha wanalipa kodi ipasavyo na wanadai risiti kila wanaponunua bidhaa na kwamba Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kukabiliana na mianya yote ya upotevu na matumizi mabaya ya fedha za Serikali.
Rais Magufuli amewataka wananchi hao kuhifadhi mazingira kwa kujiepusha na vitendo vya ukataji miti katika maeneo ya hifadhi na kupunguza idadi kubwa ya mifugo inayozidi uwezo wa maeneo ya malisho waliyonayo na amekataa ombi la wananchi wa Kijiji cha Isawima waliotaka kuongezewa eneo la Kijiji hicho kwa kilometa 20 zaidi kuingia hifadhini.