Mwanamuziki wa Pop nchini Marekani, Justin Bieber amepigwa marufuku kutumbuiza nchini China kutokana na utovu wa nidhamu.
Taarifa iliyotolewa na wizara Utamaduni nchini humo imesema kuwa haifai kwa watumbuizaji ambao wamejihusisha katika “utovu wa nidhamu” kuruhusiwa kuingia nchini humo.
Taarifa hiyo imetolewa kujibu swali lililokuwa limeulizwa na mmoja wa watu katika tovuti ya wizara hiyo.
Taarifa hizo zimetolewa baada ya wizara hiyo kujibu maswali kuhusu shabiki mmoja aliyeshangaa ni kwa nini hakuna ukumbi hata mmoja umetajwa kuwa utakuwa mwenyeji wa Bieber ilhali anatarajiwa kuanza ziara yake Asia karibuni.
Bieber aliwahi kuzuru China mwaka 2013, lakini sasa amejiunga na orodha ndefu ya wanamuziki waliopigwa marufuku nchini humo.
Wengine ni bendi ya Uingereza kwa jina Oasis na kundi la Marekani kwa jina Maroon 5, ambao wamepigwa marufuku kwa sababu ya misimamo yao ya kisiasa badala ya tabia.
Mwaka 2014, Bieber, maarufu kwa wimbo wake Sorry alizua utata baada ya kuweka picha aliyopigwa akitembelea madhabahu ya Yasukuni jijini Tokyo.
Madhabahu hayo nchini Japan yalijengwa kwa heshima ya wanajeshi waliouawa vitani pamoja na wahalifu wa kivita lakini nchini China na Korea Kusini, hutazamwa kama ishara kwamba Japan haijajutia makosa yaliyotendwa na watawala wa nchi hiyo China na Japan miaka ya nyuma.