Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kusimamia biashara ya mazao mbalimbali katika maeneo yao ili wakulima waweze kupata tija.
Pia amesema Bodi ya Mazao Mchanganyiko inazunguka nchi nzima kupata taarifa za bei ya mazao hayo ili kujirisha iwapo wanunuzi wa mazao mchanganyiko ya wakulima kama wananunua kwa bei inayostahili.
Alitoa agizo hayo jana wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ilasilo kilichoko katika mpaka wa mkoa wa Mbeya na Songwe alipokuwa njiani kuelekea wilayani Songwe kwa ajili ya ziara ya kikazi.
Alisema kwa sasa bodi hiyo inazunguna nchini kote kutafuta taarifa za bei za mazao ili kubaini bei zinazotumiwa na wanunuzi wa mazao hayo kama zinastahili baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wakulima wa eneo hilo.
Pia Waziri Mkuu aliwaagiza watu wote wanaohusika na suala la usambazaji wa pembejeo kuhakikisha wanazifikisha kwa wakulima katika kipindi kisichopungua muda wa miezi miwili kabla ya kuanza kwa msimu ili kuwaondolea changamoto ya uchelewashwaji wa huduma hiyo.